Matthew 5:12-46

12 aFurahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo walivyowatesa manabii waliokuwa kabla yenu.

Chumvi Na Nuru

(Marko 9:50; Luka 14:34-35)

13 b “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu chochote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu.

14 c “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika. 15 dWala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliyemo ndani ya ile nyumba. 16 eVivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

Kutimiza Sheria

17 f “Msidhani kwamba nimekuja kufuta Sheria au Manabii; sikuja kuondoa bali kutimiza. 18 gKwa maana, amin nawaambia, mpaka mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yoyote kutoka kwenye Sheria, mpaka kila kitu kiwe kimetimia. 19 hKwa hiyo, yeyote atakayevunja mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri hizi, naye akawafundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni, lakini yeyote azitendaye na kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika Ufalme wa Mbinguni. 20 iKwa maana nawaambia, haki yenu isipozidi haki ya Mafarisayo na walimu wa sheria, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni.

Kuhusu Hasira

(Luka 12:57-59)

21 j “Mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiue. Yeyote atakayeua atapaswa hukumu.’ 22 kLakini mimi nawaambia kwamba, yeyote atakayemkasirikia ndugu yake, atapaswa hukumu. Tena, yeyote atakayemwambia ndugu yake, ‘Raka,’
Raka ni neno la Kiaramu ambalo maana yake ni dharau au dhihaka ya hali ya juu.
atapaswa kujibu kwa Baraza la Wayahudi.
Baraza la Wayahudi lilikuwa kundi kuu kabisa la utawala wa Wayahudi lililoundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu.
Lakini yeyote atakayesema ‘Wewe mpumbavu!’ atapaswa hukumu ya moto wa jehanamu.

23 n “Kwa hiyo, kama unatoa sadaka yako madhabahuni, ukakumbuka kuwa ndugu yako ana kitu dhidi yako, 24 oiache sadaka yako hapo mbele ya madhabahu. Enda kwanza ukapatane na ndugu yako; kisha urudi na ukatoe sadaka yako.

25 p “Patana na mshtaki wako upesi wakati uwapo njiani pamoja naye kwenda mahakamani, ili mshtaki wako asije akakutia mikononi mwa hakimu, naye hakimu akakutia mikononi mwa askari, nawe ukatupwa gerezani. 26Amin, nakuambia, hautatoka humo hadi uwe umelipa senti ya mwisho.

Kuhusu Uzinzi

27 q “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Usizini.’ 28 rLakini mimi nawaambia kwamba, yeyote amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. 29 sJicho lako la kuume likikusababisha kutenda dhambi, lingʼoe ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima ukatupwa jehanamu. 30 tKama mkono wako wa kuume ukikusababisha kutenda dhambi, ukate, uutupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima utupwe jehanamu.

Kuhusu Talaka

(Mathayo 19:9; Marko 10:11-12; Luka 16:18)

31 u “Pia ilinenwa kwamba, ‘Mtu yeyote amwachaye mkewe sharti ampe hati ya talaka.’ 32 vLakini mimi nawaambia, yeyote amwachaye mkewe isipokuwa kwa kosa la uasherati, amfanya mkewe kuwa mzinzi. Na yeyote amwoaye yule mwanamke aliyeachwa, anazini.

Kuhusu Kuapa

33 w “Tena mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiape kwa uongo, bali timiza kiapo kile ulichofanya kwa Bwana.’ 34 xLakini mimi nawaambia, msiape kabisa: iwe kwa mbingu, kwa kuwa ni kiti cha enzi cha Mungu; 35 yau kwa dunia, kwa kuwa ndipo mahali pake pa kuwekea miguu; au kwa Yerusalemu, kwa kuwa ndio mji wa Mfalme Mkuu. 36Nanyi msiape kwa vichwa vyenu, kwa kuwa hamwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. 37 z‘Ndiyo’ yenu iwe ‘Ndiyo,’ na ‘Hapana’ yenu iwe ‘Hapana.’ Lolote zaidi ya hili latoka kwa yule mwovu.

Kuhusu Kulipiza Kisasi

(Luka 6:29-30)

38 aa “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’ 39 abLakini mimi nawaambia, msishindane na mtu mwovu. Lakini kama mtu akikupiga kwenye shavu la kuume, mgeuzie na la pili pia. 40 acKama mtu akitaka kukushtaki na kuchukua joho lako, mwachie achukue na koti pia. 41 adKama mtu akikulazimisha kwenda maili moja, nenda naye maili mbili. 42 aeMpe yeye akuombaye, wala usimgeuzie kisogo yeye atakaye kukukopa.

Upendo Kwa Adui

(Luka 6:27-28, 32-36)

43 af “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’ 44 agLakini ninawaambia: Wapendeni adui zenu na waombeeni wanaowatesa ninyi, 45 ahili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. 46 aiKama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo?
Copyright information for SwhNEN